Leviticus 11:2-23

2 a“Waambieni Waisraeli: ‘Kati ya wanyama wote waishio juu ya nchi, hawa ndio mtakaowala: 3Mwaweza kula mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili na ambaye hucheua.

4“ ‘Kuna wanyama wengine ambao hucheua tu au wenye kwato zilizogawanyika tu, lakini hao kamwe msiwale. Ngamia ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; kwa kawaida ya ibada hiyo ni najisi kwenu. 5Pelele ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu. 6 bSungura ingawa hucheua hana kwato zilizogawanyika; huyo ni najisi kwenu. 7 cNaye nguruwe ingawa anazo kwato zilizogawanyika sehemu mbili, hacheui; huyo ni najisi kwenu. 8 dKamwe msile nyama yao wala kugusa mizoga yao; wao ni najisi kwenu.

9“ ‘Kuhusu viumbe wote wanaoishi ndani ya maji ya bahari na vijito, mtakula wale wote wenye mapezi na magamba. 10 eLakini viumbe wote ndani ya bahari au vijito wasio na mapezi na magamba, wakiwa miongoni mwa makundi au viumbe wote ndani ya maji, hao ni machukizo kwenu. 11 fNao watakuwa machukizo kwenu. Msile nyama yao, nayo mizoga yao itakuwa machukizo. 12Chochote kinachoishi ndani ya maji ambacho hakina mapezi na magamba kitakuwa chukizo kwenu.

13 g“ ‘Wafuatao ndio ndege watakaokuwa machukizo kwenu, hivyo msiwale kwa sababu ni chukizo: tai, furukombe, kipungu, 14 hmwewe mwekundu, aina zote za mwewe mweusi, 15 iaina zote za kunguru, 16mbuni, kiruka-njia, dudumizi, kipanga, shakwe, aina zote za kipanga, 17bundi, mnandi, bundi mkubwa, 18 jmumbi, mwari, nderi, 19 kkorongo, koikoi wa aina yoyote, hudihudi na popo.

20 l“ ‘Wadudu wote warukao ambao hutembea kwa miguu minne watakuwa chukizo kwenu. 21Lakini wako viumbe wenye mabawa ambao hutembea kwa miguu minne mtakaowala: wale wenye vifundo katika miguu yao ya kurukaruka juu ya ardhi. 22Miongoni mwa hawa, mtakula nzige wa aina zote, senene, parare au panzi. 23Lakini viumbe wengine wote wenye mabawa na wenye miguu minne ni machukizo kwenu.

Copyright information for SwhNEN